Katika ziara ya mwisho ya Hekalu , Yesu alisema :mtoleeni kaisari vilivyo vya kaisari na mtoleeni Mungu vile vilivyo vya Mungu (Marko 12:17), maneno hayo yanatenganisha Imani ya kidini na madaraka ya kisiasa , lakini katika muda wa mwaka mmoja tu baada ya kupata madaraka ya kisiasa mwaka 312, Kabila la kikristo likagawanyika katika madhehebu , Kwa zaidi ya miaka 300 wakristo walidhulumiwa na kustawi , lakini mara baada ya Constantine kutanasari kanisa likakabili Utengano wa maruhubani , mafarakano ya kidona na uzushi wa Ki-Arian .Katika historia nzima ya kanisa la kikristo , uzushi ama kutengana na Imani halisi ya kanisa ndilo jambo litiwalo umuhimu Sana.
Mkutano mkuu wa kwanza wa maaskofu wote wa kanisa ulifanyika mwaka 325 huko Bithynian Nicea na ukatoa kanuni ya Imani kuhusu utatu, Arius ambaye hakutubu akalaaniwa na mkutano na kufukuzwa nchini na Mfalme Constantine. Mfalme aliamuru pia vitabu vyote vya Arius vichomwe moto na mwenye kuwa navyo apewe adhabu ya kifo.
Duara la Uhuru wa dini lililoanzia kwa Yesu wa Nazareth likakamilika wakati wa utawala wa Justinian (483-565) alipoamuru kwamba mwenye kuacha dini auawe, adhabu hiyo ikawa sehemu ya kanuni katika Sheria ya Rumi mnamo mwaka 535 AD. ni bahati mbaya sana kwamba Uhuru wa mawazo ulifutiliwa mbali na wakristo wa Rumi ambao Babu zao waliotanasari muda mchache uliopita walichomwa moto huku wakifurahiwa wakati wa Rumi ya Nero (64 AD).
Kwa muda wote wakristo walikuwa wanadhulumiwa na wenye madaraka ya kisiasa na wasiokuwa wakristo , waandishi wa kikristo walipigania Uhuru wa dini , lakini pindi kiti cha kifalme kiliponyakuliwa na ukristo , Kanisa lilianza kuona Uhuru wa mtu binafsi katika Imani ,kwa jicho la uhasama Serikali iliutupia jicho utengano au uasi huo.
Katikati ya Karne ya tano, vitu vilivyokuwa vya Mungu na bado ni vya Mungu vilitolewa kwa kaisari , utawala wa kisiasa ukawa mkono wa kuume wa kanisa . Mt Augustino (354-430) katika juhudi zake dhidi ya Ma-Donatisti alihoji "Yapo mateso ya haki ambayo kanisa la Yesu linawatesa watu kwa mapenzi mema ili kuwasahihisha kwa kuwatoa katika makosa , kuwachukulia hatua kwa wema wao, ili kuhifadhi wokovu wao wa milele.
Mnamo mwaka 385 Askofu mmoja wa Uhispania , jina lake Priscilian alishtakiwa kwa kuhubiri kwamba, shetani na mungu wapo pamoja siku zote akawa anahubiri useja kwa watu wote, yeye alikataa shitaka , lakini alihukumiwa na kupewa adhabu ya kufungwa kwenye mti na kuchomwa moto pamoja na wafuasi wake wengi.
Martin Luther (1483--1546) kiongozi Mjerumani wa kanisa la Protestant Reformation , alikubaliana na mtangulizi wake mkatoliki wa Rumi, Augustino na akasema :wenye madaraja katika kanisa Wana madaraka juu ya dhamiri za watu , lakini imeonekana ni lazima waungwe mkono na utawala kwa kutoa adhabu maalum ya uharamia ili mradi kosa lifutiliwe mbali ijapokuwa kuondoa dhambi ni Jambo lisilowezekana.
Mtaalamu wa dini aliyekuwa Mprotestanti Mfaransa , John Calvin (1509--64) ndiye aliyeeneza dini kwa upanga katika utawala wake na kuweka kifo kuwa adhabu ya kuacha dini ,Alidai Wakatoliki wanapaswa kupewa zile adhabu wanazopewa wale wanaochochea fitina ya kuasi Serikali.
Lakini mtu aliyeitwa Thomas Hobbes (1588--1679) katika kitabu chake Cha 'Leviathan' anapingana na Calvin na kudai kuwa, kwa kuwa uwezo wa kuonyesha miujiza ndio alama mojawapo ya Nabii mkweli, Hobbes anasisitiza kwamba siku za kuonyesha miujiza zimekwisha malizika zamani , hivyo hakuna uwezekano wa kupata mwongozo kwa njia ya unabii.
Nguvu za kisiasa zinafanya kazi kwa kuvaa mavazi ya Kiislamu , mara nyingi wanaofanya hayo na kujifaidisha nayo sio waislamu wenyewe, Mtume s.a.w aliruhusiwa kutangaza dini na kueneza ujumbe wa Mungu kwa amani , watu wa Makkah hawakumpa Uhuru huo na wakawaadhibu walioanza kumwamini yeye, wengi waliacha dini zao za asili na kusilimu na kuacha kuabudu masanamu.
Mtawa mmoja wa kireno alisilimu lakini baadaye akarejea katika Imani yake ya zamani , yeye akauawa Mjini Aurangabad , Sababu za kuuawa kwake zilikuwa za kisiasa si za kidini, Yeye alishukiwa sana kuwa ni jasusi wa Kireno aliyesilimu ili asijulikane kwamba anafanya uchunguzi
Jadd bin Dirham aliuawa kwa amri ya Hisham bin Abdul Malik huko Kufa au Waist, mnamo mwaka 124 au 125 Hijriyyah/AD 746 au 747 alishtakiwa kueneza itikadi ya Kimutazila kuhusu kuumbwa kwa Kurani na Uhuru wa mawazo, mwaka 167 au 168 Hijriyyah/AD 788.
Mshairi wa Iraq , Bashir bin Burd aliuawa baada ya kushtakiwa kwa uzandiki , akapigwa na kutupwa katika bwawa la Batiha. Husain bin Mansur Hallaj aliuawa mnamo mwaka 309 Hijriyyah/930 AD kwasababu ya kudai ameungana na Mungu sana tena mno hata kwamba amezama ndani ya Mungu.
Shihabud Din Suhrawardi naye aliuawa kwa amri ya Malik Dhahir (578 Hij./1199AD) kwa hatia kwamba aliamini Kila kitu kilicho hai, kitembeacho ama kinachokuwepo kuwa ni ukweli hata akaweka msingi wa uhakikisho wake wa Mungu juu ya alama ya Nuru.
Shahidi wa Karne ya kumi na saba alikuwa Muhhamad Said Sarmad, yeye alizaliwa huko Kashan kwa wazazi wake waliokuwa wayahudi , naye alikuwa Rabbi (Mwalimu wa Kiyahudi) kabla hajasilimu , yeye aliamini kuwepo kwa dhati moja pekee na akakataa kuwepo kwa vitu vyote vingine ,Yeye aliuawa katika enzi ya Aurangabad (alitawala 1658--1707 )Kaburi lake linatazamana na Jami 'Masjid wa Delhi na linavutia mamia ya watu Kila Siku ambao huweka hapo mashada ya maua na kusoma Fatiha.
Muhammad Mahmud Taha aliuawa huko Sudan mwaka 1985 ,yeye aliamini kwamba Sheria ya Kiislamu iliyomo katika sura zilizoteremka Madina hazina kazi tena.
Sultani wa ki-uthmani , kiongozi wa ufalme wa kidini na khalifa wa waislamu kwa ujumla , hakuamuru kumwua Baha-Ullah (1817-92) kwasababu ya kuacha dini na kurudia ile ya asili, Baha ullah alijitangaza kuwa yu aliyeahidiwa ambaye alibashiriwa na Bab, na akaanzisha Ubahai kuwa dini Mpya, Ubahai ulikuwa na mpaka Sasa ni dini iliyo kinyume na uislamu , Dini hiyo inatangaza kwamba ujaji wa Baha ullah umefutilia mbali Kurani na mafunzo ya Mtume s.a.w.
Baha ullah alitiwa jela katika Akka (Acre) karibu na Haifa, Palestina (Sasa Israel) .Lakini Sabbatai Zevi (1627-76) Sufi wa kiyahudi , alipodai kuwa yeye ni Masihi mnamo mwaka 1648 ,sheikh-ul-Islam wa ufalme wa ki-uthmani alitoa amri kwamba auawe, Basi akakamatwa , lakini akaacha madai yake ili asalimike. Baha ullah alidai kuwa yeye ni onyesho jipya la Mungu na baadae akaja kuuacha uislamu , lakini hakuuawa kwasababu aliacha dini ,bali kwasababu yeye hakuwa hatari kwa amani katika ufalme wa ki-uthmani.
Ni kwamba Mtume s.a.w. alipigana kuimarisha Uhuru wa dhamiri ; katika muda usiokuwa wa miaka miwili
baada ya Mtume kuhamia Madina ,wafuasi wake waliwakabili watu elfu moja wa Makkah waliofunga kabisa nia ya kuangamiza uislamu, Mtume wake na wafuasi wake,Ilikuwa asubuhi ya ijumaa ,tarehe 17 Machi 623 (17 Ramadhan 2 A.H ) ambapo watu wa Makkah pamoja na ngamia 700 na Askari 100 wapanda farasi walianza kuteremkia bonde la Badr kutoka mtelemko wa Aqanqal ,maili 20 upande wa kusini mwa Madina.
waislamu waliokuwepo hapo ili kuutetea uislamu walikuwa 313 pekee ,walikuwa na farasi wawili na slaha haba kabisa hata kwamba upanga wa Ukkasha ulipovunjika katika Vita, Mtume akaweza kumpa rungu badala ya upanga naye akalitumia rungu hilo katika Vita, Hali ya waislamu ikawa mbaya Sana mno, hata kwamba Mtume akapaza sauti akisema "E Allah ,Kama Kundi hili dogo la waislamu litaangamia leo ,hakuna atakayebakia ili kukuabudu!"
waislamu wakajitetea vizuri dhidi ya jeshi bora la Makkah lililokuwa na silaha nyingi za kutisha. Historia ya uislam imehifadhi majina yote ya masahaba 313 wa Mtume walioutetea uislamu katika bonde la Badr , Miongoni mwao alikuwepo Abu Bakr, Umar, Uthman, na Ali. ambao wakawa makhalifa wake baada ya Mtume kufariki.
Masahaba wakubwa watatu waliopigana baadae kwa ushujaa Sana ili kuutetea uislamu walikuwa;Sa'd bin Abi Waqqas, Abu 'Ubaidah bin Jarrah na Khalid bin Walid, hakuna Kati yao aliyesilimishwa kwa nguvu, Mamia ya wahamiaji (Muhajirin) na maelfu ya Maansar walisilimu na kumpa kimbilio Mtume aliyekuwa amedhulumiwa.
Hakuna upanga wowote uliotumika kuwasilimisha wao, Kabla hajafika Muhammad bara la kiarabu lilikuwepo na kuwa eneo la kisiasa tu Kama Kama anavyoeleza Will Durant ,kwamba "Katika kutoa majina kwa wagiriki ,wakazi wote wa bara la kiarabu waliitwa Sarakenoi ,neno ambalo linatokana na neno la kiarabu Sharqiyyun, yaani watu wa Mashariki , mwanzo waliitwa 'Scenite Arabs' yaani Waarabu walioishi katika mahema (kutokana na neno la kigiriki skene ,hema).
Waliishi katika nchi kame ,walijitegemea kikabila ,Katika muda wa miaka elfu ya pili kabla ya Yesu, Waarabu walifuga ngamia mnyama anayelingana kabisa na maisha ya jangwani, Maziwa yake walitumia kuwa riziki na mkojo wake kuwa tiba, Nyama yake ndiyo laini na ngozi yake na manyoya yake vilitumika kuwa mavazi .
Hata mavi yake yaliweza kutumika kuwa kuni ,Ngamia aliweza kutembea kwa Siku 25 katika kipupwe bila kupata maji na Siku tano katika kiangazi , vikundi vya mabedui viliwafuata ngamia zao, ngamia wakiwa Mali kwao ,Aloy Sprenger akielezea historia ya mabedui wa kiarabu wa kabla ya uislamu aliwaita 'Wadusi wa ngamia".
Mwarabu hakutambua wajibu wa kuwa mwaminifu kwa Kundi lolote kubwa kuliko kabila lake mwenyewe, lakini mkazo wake wa kujitolea kwake ulikuwa mbalimbali kinyume cha mipaka yake, kwa ajili ya kabila lake angeweza kufanya kusudi yale yote ambayo waliostaarabika wanafanya kwaajili ya nchi yao au dini ama taifa lao, yaani kuongopa, kuiba,kuua,na Kufa.
Hakulazimishwa na Sheria yoyote iliyopo katika maandishi ,wala hakuna Serikali iliyokuwepo kuweka Sheria, waarabu walisikitikia kuzaliwa kwa mabinti na wakajificha kwa sababu ya kuona aibu na kufedheheka ,Pengine mabinti waliuawa palepale walipozaliwa tu.
Kama walinusurika kuuawa uzuri wao wa maumbile ukasababisha wakapendwa na waume zao ama wapenzi wao ambao wangetia Kila juhudi na kufanya juu chini ili kulinda heshima zao kina mama hao. lakini hawakuthaminiwa zaidi ya mali na vyombo, walikuwa ni Mali za baba zao ,waume wao ama Wana wao na walirithiwa pamoja na vyombo vingine na mali alizoacha marehemu ,walikuwa ni watumwa tu na kwa nadra walipata kuwa rafiki wa baba zao ,waume wao ama ndugu zao.
mwarabu alifikiria kidogo Sana maisha ya akhera ,Alitoa dhabihu ya binadamu ,aliabudu mawe "matakatifu" Makao Makuu ya ibada ya mawe hayo yalikuwa ni Makkah, Kabla ya ujaji wa uislamu,ndani ya Ka `ba mlikuwapo na masanamu mengi Sana yaliyohesabiwa kuwa miungu ,Sanamu moja la akiki liitwalo Hubal lilikuwa ni Mungu mkubwa wa Makkah .
Lakini katika Hijaz masanamu matatu Lat ,Manat, na Uzza, yalikuwa ni fahari ya huko kuwa binti wa Mungu.
Mwarabu alikuwa ni mtu madhubuti na mwenye nguvu nyingi na aliweza kuishi kwa kutumia tende chache na maziwa kidogo ya ngamia. kutokana na mtende alitengeneza kileo kilichompandisha juu kimawazo ya kishairi na mapenzi. Maisha yake yalikuwa mara ya kimapenzi mara ya kivita, mwarabu alikuwa anaharakia Sana kujilipiza kisasi Cha kufedheheshwa na kuheruhiwa, si kwaajili yake tu bali na kwa niaba ya kabila lake pia.
Jicho kwa jicho na jino kwa jino ilikuwa ni Sheria , Kama mtu hakuweza kumwua aliyemuudhi , mtu huyo alipata fedheha Sana ya kudumu dawamu , sehemu kubwa ya maisha yake ilikuwa inapita katika kulipiza kisasi cha kabila lake , Katika Zama za kabla ya historia, jina 'Ayyamul Arab (Siku za waarabu) lilimaanisha Vita vya waarabu baina yao wenyewe, Baadhi ya Siku za Vita zilikuwa maarufu , kwa mfano siku ya Buath ama siku ya Fijar.
Mara nyingi uhasama huo baina ya makabila ulisababishwa na ugomvi kuhusu mifugo , ardhi na chemchem. Mapigano mashuhuri Sana Miongoni mwa mapigano ya aina hiyo ndio yaliyopatikana baina ya makabila ya Bani Bakr na jamaa zao Banu Taghlib na sababu yake ilikuwa ni ngamia mmoja jike wa mama mmoja wa mzee wa kabila la Banu Bakr aitwaye Basis, Mtemi mmoja wa Banu Taghlib akawahi kumjeruhi huyo ngamia , Jambo lililosaba isha mapigano yaliyoendelea miaka arobaini , mapigano hayo yalimalizika kwasababu ya makabila yote hayo mawili kuishiwa nguvu , Hayo mapigano ya Basus yalipomalizika tu Vita nyingine ikaanza iitwayo Siku ya Dahis na Gharba,.
Sababu ya Vita hiyo ilikuwa ni mienendo isiyo sawa ya watemi wawili katika shindano la mbio za farasi dume aitwaye Dahis na farasi jike Gharba, Vita hiyo iliendelea kwa makumi ya miaka, hayo yalikuwa mazingira ya maisha ya jamii ambamo Mtume Muhammad alikulia, na hao walikuwa watu ambao Mungu aliwapa kwanza nafasi ya kuungana na Imani ya Mtume aliyedhulumiwa kwa sababu ya dini.
kusema kwamba watu hao waarabu wakali na wapenda Vita waliokuwa tayari kupigana kwasababu ya Jambo dogo kabisa wangeliweza kusilimishwa kwa nguvu ndiyo kuharibu historia, Katika historia ya dini ya kikristo inaonekana ikizigeuza panga kuwa vyombo vya kilimo ,
Watu wanaotumia mabavu kwa jina la dini kwakweli hawatambui kabisa kiini Cha dini , Dini huhusika na moyo , Dini siyo siasa, na watu wa dini hawaundi vyama vya siasa , hilo ni badiliko la moyo badiliko kwa wema wa roho, makao ya dini ndiyo undani wa moyo, ni mbali na utawala wa upanga, milima haiondolewi na upanga wala mioyo haigeuzwi na nguvu, japokuwa kutumia mabavu kwa jina la dini ndilo Jambo linalokaririwa katika historia ya ukatili wa mtu,
Manabii laki moja na elfu ishirini na nne walitumwa na Mungu ambao walionyesha kwa mafunzo yao na matendo yao kwamba ni wenye kuleta ujumbe wa Mungu ,ndio wanaokandamizwa na kudhulumiwa na sio wenye kukandamiza na kudhulumu, Manabii walishinda nyoyo kwa hulka njema na nguvu ya kiroho. si kwa nguvu ya kimwili . Ni sikitiko kubwa kwamba mapadre waliotawazwa na masheikh wenye vilemba waliovaa majoho ya utawa ndio waliowadhulumu wasio na hatia kwa jina la Manabii ambao wenyewe walidhulumiwa.
Kwa nguvu walishika madaraka yote kuhusu mambo ya dini ilhali hawakujua dini ni kitu gani, walidai kulinda heshima ya manabii wao kwa njia ya kuwadhuru wengine, na kueneza uwongo kwa nia ya kuudhi, na kwa kutenda matendo ya kikatili kinyume cha ubinadanu , Walifanya hivyo kabla ya Mtume s.a.w na bado wanatenda vivyo hivyo hata Sasa.
Katika Zama za kale wafuasi hao wa jina tu, wa Yesu -mapapa na maaskofu , makadinali , na makasisi , na wazee wa kanisa , waliandika katika historia mlango wa vitisho , Mt Augustino akayaita hayo kuwa mabavu mema wanayofanyiwa wapotovu, Katika kanisa la Yesu leo, wanahistoria wa kikristo wanakubali kwamba 'mabavu mema' hayo yaliyofanywa kwa jina la Yesu ndiyo aibu kwa kanisa.
katika jumba la masanamu yaliyotengenezwa na nta la Mama Tussaud huko London, mabavu hayo ya ajabu yenye kuhuzunisha na kutisha yameonyeshwa , na mtu anaweza kuyaona maonyesho hayo huko. Jumba hilo la kuhifadhi vitu vya kale lilianzishwa kwanza mjini Paris mnamo mwaka 1770 Kisha likahamishwa mwaka 1802 na kupelekwa Uingereza.
Kwenye kuta zake yametengenezwa masanamu ya watu wakubwa maarufu na watu waovu . chumba chake Cha "Matisho" (Chamber of Horrors) ni namna ya Gereza chini ya ardhi , Masanamu hayo yametengenezwa kwa ufundi na umahiri hata kwamba yanaonekana si masanamu bali ni watu wazima hasa, wageni wengi humo wakati mwingine wanamwomba mwangalizi wa jumba hilo mwenye uso wa kirafiki kuelekezwa, kumbe mwangalizi huyo ni sanamu tu! Yapo maonyeshoni humo masanamu yaliyotengenezwa na Mama Tussaud mwenyewe kutokana na vichwa vilivyokatwa vya Louis XIV na Marie Antoinette.
Pia Kuna miti ya kunyongea Ile asilia pamoja na vyombo vya kutesea Kama vile mkatale wa kufungia kichwa na mikono, Mkatale wa kufungia mikono na miguu , mti wa kufungia watu wachapwe mijeledi , kiti cha kufungia watu ili kuwazamisha majini na kuwatoa mara kwa mara ili kuwaadhibu , kitanda cha chuma cha kushtusha viungo vya mtu kwa kumtesa ,Magari (Galleys) kitanda cha Procrustes (Cha kumfunga mtu ili kumtesa) msalaba , miti ya kunyongea , tanzi la roho na vingine vingi, vyombo vingine ni vya kuogofya mno kwamba vimefunikwa ili watoto na wengine wenye udhaifu wa moyo wasiweze kuviona,
Vyombo vya kutesea vilivyomo katika jumba la Mama Tussaud vinaelezea habari za kutisha za mabaraza ya Uhispania na Ufaransa walimohukumiwa kimabavu wale waliohitilafiana na wakuu wa dini katika masuala ya dini , waliteswa na kusumbuliwa kwasababu eti wameacha dini ya kimapokeo na kubadili dini , walilazimishwa kukiri kwamba wameachana na dini ya kweli , walipokataa wakachapwa na kupigwa mijeledi, wakalazwa juu ya kitanda cha kushtusha viungo vya mwili, au kuhukumiwa kifo, wakachomwa na mikuki , wakatiwa kwenye Mkatale, wakachomwa na chuma cha moto ama wakachomwa moto kabisa. watesaji hawa wanamkumbusha mtu mateso ya Yesu alipowekewa taji la miiba na kusurubiwa msalabani Golgotha.
Kanuni ya kutokulazimishana katika Mambo ya dini ilirudiwa kutangazwa baada ya ushindi katika Vita ya Badr (Kurani 3:21) na Tena katika Sura Al-Maidah (Sura ya 5) ambayo ndio sura ya mwisho kufunuliwa, Sasa baada ya madaraka ya Mtume s.a.w kuimarika kikamilifu ,si tu katika Madina bali huko Makkah pia, ilikuwa kazi ya kukazania na kusisitiza kwamba wajibu hasa wa Mtume s.a.w ulikuwa ni kufikisha tu ujumbe wa Allah, Basi "Mtiini mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na mjihadhari ,lakini mkigeuka ,basi jueni ya kwamba juu ya Mtume wetu ni kufikisha tu ujumbe waziwazi.(5:93) na mwishowe "Hakuna juu ya Mtume ila kufikisha tu ujumbe na mwenyezi Mungu anajua mnayoyadhihirisha na mnayoyaficha (5:100) Imani ya kidini ni kitu cha mtu binafsi, siyo Serikali ama wakuu wa dini bali ni Mungu pekee anayejua anayodhihirisha mtu ama anayoyaficha.
Historia ya kidini imejaa mifano mingi ya kutumia nguvu na jefule kwa jina la dini, mfano utawala wa Taleban uliochukua madaraka Afghanstan hivi karibuni, umeanzisha na kuunga mkono adhabu zinazoendana na dini ya Kiislamu kama vile hukumu ya mauaji hadharani kwa walioshitakiwa kwa mauaji au uzinifu na kukatwa mikono kwa waliopatikana na hatia ya wizi. wanawake wakitakiwa kuvaa Burka vazi linalofunika uso baadhi inasemekana waliuawa kwa kutovaa Burka.
Lakini watu wengi katili utakuta hawana dini, watu walidhulumiwa kwa jina la Mungu na wale ambao hawana habari ya Mungu hata kidogo. Nabii Nuhu aliyewaita watu wake kwenye kumcha Mungu na utakaso hakutumia nguvu, wale waliotaka kuzima sauti yake walikosea ,waliposikia ujumbe wa Nabii Nuhu wakasema "Kama hutaacha ,ewe Nuhu ,bila Shaka utakuwa miongoni mwa wanaorujumiwa.(26:117).
Wafuasi wa dini ya kweli hupata kuteswa, mfano ,Nabii Ibrahimu aliwaita watu kwa Mungu kwa njia ya upendo, huruma na unyenyekevu ,Hakuwa na upanga mkononi, Hakuwa na silaha ya aina yoyote, lakini wazee wa kaumu yake walimtendea kama walivyotenda wapinzani wa Nabii Nuhu wapingao dini. Babake Ibrahimu ,Azar ,alisema :"Kama huachi lazima nitakupiga mawe " (19:47) Maneno aliyotamka Azar yalikuwa ni yaleyale yaliyotamkwa na maadui wa Nabii Nuhu. Manabii wote wawili Nuhu na Ibrahimu, walifedheheshwa na kudhalilishwa ,wote wawili walipigwa na kuteswa ,lakini wote wawili waliyavumilia hayo kwa subira ,wakiisha washa moto wa dhuluma na fitina wasumbufu hao wakajaribu kumchoma moto Ibrahimu akiwa hai.
Wale waliompinga Nabii Luti hawakuijua dini kabisa ,hata hivyo walikuwa maadui zake na wafuasi wake kwa jina la dini. Walimtisha kwamba watamtesa ,walimwonya yeye na wafuasi wake kwamba watafukuzwa, Walifanya juu chini ili kumkomesha asihubiri dini yake.
Watu wa Nabii Shuaibu walifanya hivyo hivyo na wakasema "Tutakutoa wewe na wale walioamini pamoja nawe katika mji wetu au huna budi kurudi katika Mila yetu(7:89). Nabii Musa na wafuasi wake waliteswa vilivyo na waliojifanya viongozi wa dini wa Zama hizo, Firauni ,Hamana na Karuni, waliosema :"waueni watoto Wanaume wa wale walioamini pamoja naye na waacheni hai wanawake wao(40:26) .
Manabii hawakuwaadhibu watu kwasababu tu walibadili dini ,hata hivyo manabii na wafuasi wao waliadhibiwa kwa kusingiziwa wamekufuru ,baada ya Musa , Yesu alivumilia mateso na ukatili wa aina hiyo hata kwamba wakajaribu kumwua msalabani . Siku zote damu ilimwagwa na watu wakateswa kwa jina la dini na hao walioudhiwa Kila mara, ndio waliohukumiwa kuwa wamejitoa katika dini .hata hivyo hakuna kitabu hata kimoja kinachoruhusu kuwaadhibu watu wanaobadili dini yao.
Wakristo waliwahi kuteswa katika pango kwa miaka 300, viwanja vya michezo Kama wanavyocheza Simba na yanga leo au maeneo ambayo wapiganaji hupigana na mafahali ya Simba ,katika viwanja hivyo wakristo Zama za dola za kirumi wakiwa uchi wa mnyama walitupwa kuliwa na wanyama wa porini wenye njaa, wanyama hao wakalia na kuwamaliza haraka wakristo hao wasioweza kujitetea .
Wakati mwingine hao walioacha dini wakatupwa mbele ya mafahali walionyimwa kujilisha kwa Siku nyingi ,wanyama hao wenye njaa Kali wakalia na kuunguruma kuwashambulia wakristo hao na kuwapiga pembe zao na kuwakanyaga chini ya miguu, hata baadae maskini hao wakafa, na baada ya sherehe hiyo ya mauaji Warumi wachekao wakarejea nyumbani wakifurahia ,
Mateso hayo yaliendelea kwa Karne tatu katika vipindi . Na walipokosa kujitafutia popote pa kujificha wakakimbilia mapango Yale ya kuzikia watu .Mazingira hayo bado yapo hata Leo yanayotukumbusha kwamba wakristo hao waliweza kuishi pamoja na vidudu ,nge na majoka ,lakini hawakuweza kuishi na viongozi wa dini waliovaa majoho maridadi. Wapo waliokimbilia chini ya ardhi katika mapango hayo wapo wakristo wengine pia waliotajwa na vitabu vya dini kwamba waliamini Umoja wa Mungu na wakachomwa Moto wakiwa hai .
Ukristo ulishughulikia vitendo viovu vya dhuluma na mabavu , na baadhi ya wafalme wa kikristo walitenda vitendo vya kikatili na udhalimu wakiwa na fikra potofu kwamba walikuwa wanaisaidia dini ya Yesu, wakati wa Zama za kifo cheusi (Black Death) 1348-49, Wayahudi wengi walichomwa moto wakiwa hai ndani ya nyumba zao. wakati wa mabaraza ya kuwahukumu wazushi ya Uhispania na Ufaransa wanawake wengi wasio na yeyote wa kuwasaidia waliuliwa nyakati mbalimbali kwa kusingiziwa kuwa wachawi na fikra hiyo potofu ikaenea na kuwa ndiyo njia pekee ya kikristo ya kuushughulikia uchawi.
No comments:
Post a Comment